Deuteronomy 31

Yoshua Kutawala Baada Ya Musa

(Hesabu 27:12-23)

1Kisha Musa akaenda akasema maneno haya kwa Waisraeli wote: 2 a“Sasa nina miaka mia moja na ishirini nami siwezi tena kuwaongoza. Bwana ameniambia, ‘Hutavuka Yordani.’ 3 b Bwana Mwenyezi Mungu wenu, yeye mwenyewe atavuka mbele yenu. Ataangamiza mataifa haya mbele yenu, nanyi mtaimiliki nchi yao. Pia Yoshua atavuka mbele yenu, kama Bwana alivyosema. 4 cNaye Bwana atawafanyia watu hao kile alichowafanyia Sihoni na Ogu, wafalme wa Waamori, ambao aliwaangamiza pamoja na nchi yao. 5 d Bwana atawakabidhi kwenu, nanyi lazima mwatendee yale yote niliyowaamuru. 6 eKuweni imara na moyo wa ushujaa. Msiogope wala msifadhaike kwa sababu yao, kwa kuwa Bwana Mwenyezi Mungu wenu anakwenda pamoja nanyi; kamwe hatawaacha wala hatawatupa ninyi.”

7 fKisha Musa akamwita Yoshua na akamwambia mbele ya Israeli wote, “Uwe imara na moyo wa ushujaa, kwa kuwa ni lazima uende na watu hawa katika nchi ile Bwana aliyowaapia baba zao kuwapa, nawe ni lazima uwagawie kama urithi wao. 8 g Bwana mwenyewe atakutangulia naye atakuwa pamoja nawe; kamwe hatakuacha wala hatakutupa. Usiogope, wala usifadhaike.”

Kusoma Sheria

9 hKwa hiyo Musa akaandika sheria hii na kuwapa makuhani, wana wa Lawi, waliochukua Sanduku la Agano la Bwana na wazee wote wa Israeli. 10 iKisha Musa akawaamuru, akasema: “Mwishoni mwa kila miaka saba, katika mwaka wa kufuta madeni, wakati wa Sikukuu ya Vibanda, 11 jWaisraeli wote wanapokuja mbele za Bwana Mwenyezi Mungu wenu mahali atakapopachagua, utasoma sheria hii mbele yao masikioni mwao. 12 kKusanya watu wote, wanaume, wanawake, watoto na wageni wanaoishi katika miji yenu, ili waweze kusikia na kujifunza kumcha Bwana Mwenyezi Mungu wenu na kufuata kwa bidii maneno yote ya sheria hii. 13 lWatoto wao, ambao hawaijui sheria hii, lazima waisikie na kujifunza kumcha Bwana Mwenyezi Mungu wenu kwa muda mtakaoishi katika nchi mnayovuka Yordani kuimiliki.”

Kuasi Kwa Waisraeli Kunatabiriwa

14 m Bwana akamwambia Musa, “Sasa siku ya kifo chako imekaribia. Mwite Yoshua, mkajihudhurishe katika Hema la Kukutania, mahali nitakapompa maagizo ya kazi.” Kwa hiyo Musa na Yoshua wakaja na kujihudhurisha kwenye Hema la Kukutania.

15 nKisha Bwana akatokea katika Hema katika nguzo ya wingu, nalo wingu likasimama juu ya ingilio la Hema. 16 oKisha Bwana akamwambia Musa: “Unakwenda kupumzika na baba zako, nao watu hawa hivi karibuni watazini na miungu migeni ya nchi wanayoingia. Wataniacha na kuvunja Agano nililofanya nao. 17 pSiku hiyo nitawakasirikia na kuwaacha; nitawaficha uso wangu, nao wataangamizwa. Maafa mengi na shida nyingi zitakuja juu yao, nao siku hiyo watauliza, ‘Je, maafa haya hayakuja juu yetu kwa sababu Mungu wetu hayuko pamoja nasi?’ 18Nami hakika nitauficha uso wangu siku hiyo kwa sababu ya maovu yao yote kwa kugeukia miungu mingine.

19 q“Sasa ujiandikie wimbo huu,
Wimbo huu hapa ina maana wimbo wa Musa.
uwafundishe Waisraeli na uwaamuru wauimbe, ili upate kuwa ushahidi wangu dhidi yao.
20 sNitakapokwisha kuwaingiza katika nchi itiririkayo maziwa na asali, nchi niliyowaahidi baba zao kwa kiapo, nao watakapokula wakashiba na kufanikiwa, watageukia miungu mingine na kuiabudu, wakinikataa mimi na kuvunja Agano langu. 21 tMaafa na shida zitakapokuja juu yao, wimbo huu utashuhudia dhidi yao, kwa sababu hautasahauliwa na wazao wao. Ninajua lile wanaloandaa kufanya, hata kabla sijawaingiza katika nchi niliyowaahidi kwa kiapo.” 22Hivyo Musa akaandika wimbo huu siku ile na akawafundisha Waisraeli.

23 u Bwana akampa Yoshua mwana wa Nuni agizo hili: “Uwe hodari na shujaa, kwa kuwa utawaleta Waisraeli katika nchi niliyowaahidi kwa kiapo, nami mwenyewe nitakuwa pamoja nawe.”

24 vBaada ya Musa kumaliza kuandika kwenye kitabu maneno ya sheria hii kutoka mwanzo hadi mwisho, 25akawapa Walawi wale waliolibeba Sanduku la Agano la Bwana agizo hili, akawaambia: 26“Chukueni Kitabu hiki cha Sheria mkakiweke kando ya Sanduku la Agano la Bwana Mwenyezi Mungu wenu. Hapo ndipo kitakapokaa kama shahidi dhidi yenu. 27 wKwa kuwa ninajua jinsi mlivyo waasi na mlivyo na shingo ngumu. Kama mmekuwa mkiasi dhidi ya Bwana nikiwa bado niko hai na nikiwa pamoja nanyi, mtaasi mara ngapi baada ya kufa kwangu! 28 xKusanyeni mbele yangu wazee wote wa makabila yenu na maafisa wenu wote, ili nipate kusema maneno haya masikioni mwao na kuziita mbingu na nchi ili kushuhudia dhidi yao. 29 yKwa kuwa ninajua baada ya kifo changu hakika mtakuwa waovu kabisa na kugeuka kutoka njia niliyowaamuru ninyi. Katika siku zijazo, maafa yatawapata kwa sababu mtafanya maovu mbele ya macho ya Bwana, na kuchochea hasira yake kwa yale mikono yenu itakayokuwa imefanya.”

Wimbo Wa Musa

30Musa akayasoma maneno ya wimbo huu kutoka mwanzo hadi mwisho katika masikio ya kusanyiko lote la Israeli:
Copyright information for SwhKC